Social Icons

Sunday 18 March 2012

CHADEMA NA RADA UCHAGUZI MDOGO ARUMERU

Katika mikutano yao juzi na jana, Chadema kwa upande wake walitaka kukamatwa kisha kufikishwa mahakamani, wahusika wote wa ufisadi wa rada.



Meneja mwenza wa Kampeni za chama hicho jimboni Arumeru Mashariki, Vincent Nyerere, akizungumzia kurejeshwa kwa fedha za rada, alisema hoja sio kufurahia bali ni kuwafikisha mahakamani wote waliohusika na kununua rada kwa ulaghai, hivyo kujipatia mabilioni ya fedha.



“Hoja hapa sio kurejesha chenji eti zinunuwe madawati na vitabu, hoja ni hatua gani wanachukuliwa waliohusika na kununua rada ili kujipatia fedha ambazo zilisababisha watoto wao kusoma nje na watoto wa masikini kufa kwa kukosa madawa hospitali na kukaa chini?,”Alihoji Nyerere ambaye ni Mbunge wa Musoma Mjini.



Alisema ikiwa Serikali haitawakamata watuhumiwa wa ufisadi huo, basi wafungwa wote waliotiwa hatiana kwa makosa madogo madogo kama kuiba kuku, waachiwe.



Mbunge huyo pia alimgeukia Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, John Tendwa kwa kusema kwamba kiongozi huyo hana mamlaka ya kumzuia kumzungumzia baba yake,Hayati Julius Nyerere jukwaani kwani yeye si mwanafamilia bali ni msajili wa vyama.



Akizungumza katika mikutano iliyofanyika katika vijiji cha Ngarenanyuki na Msitu wa Tembo, Nyerere alisema Tendwa kama anataka awe mwanafamilia wa Nyerere kwa kuomba, afanye hivyo.



“Tendwa ni Msajili wa Vyama vya Siasa sio msajili wa koo, kama kazi ya siasa imemshinda basi awe msajili wa koo,”alisema Nyerere.



Mbunge huyo alisema alilazimika kutoa kauli nzito dhidi ya Mkapa baada ya kutoa taarifa ya uongo kuwa hamtambui kama mwanaukoo wa Nyerere.



Akizungumzia hoja ya Tendwa kuwa wakati wa kifo cha Mwalimu, yeye (Vincent) alikuwa mtoto, alimtaka Tendwa afanye uchunguzi na kuuliza wengine kwani yeye hakuwa mtoto wakati wa kifo cha Mwalimu na kwamba alikuwa na ufahamu wa kila kilichotokea wakati huo.



Ahadi za wagombea
Wakati viongozi wa Chadema na CCM wakiendelea kupimana ubavu majukwaani, wagombea wao Nassari na Sioi, sawia wameendelea kutoa ahadi za kutatua kero za wakazi wa Arumeru Mashariki ambao kilio chao kikubwa ni uhaba wa ardhi na maji kwa ajili ya matumizi ya nyumbani na umwagiliaji mashamba.



Nassari katika ahadi zake juzi na jana alisema ikiwa atachaguliwa kuwa mbuge, atapeleka hoja binafsi bungeni kudai ardhi ya Meru ambayo kwa sehemu kubwa ipo mikononi mwa walowezi wachache.



Alisema zaidi ya ekari 13,000 zinamilikiwa na watu wachache ambao wameanzisha mashamba ya maua na kujenga viwanja vya gofu na farasi, huku wakizuia maji kufika katika makazi ya watu na badala yake maji hayo, kutumika kumwagilia uwanja na kuogeshea farasi.



“Leo hii kuna mashamba ya maua hapa, licha ya kukopeshwa na Benki ya Rasilimali Tanzania (TIB) Sh50 bilioni kwa udhamini wa Serikali, wameshindwa kulipa mishahara mizuri, badala yake wanawalipa ninyi kati ya Sh53,000 na 60,000 wakati pia afya zenu zinadhurika,”alisema Nassari.



Alisema pia atahakikisha anarejesha soko la Mbuguni, kutatua tatizo la maji na afya na pia kuhakikisha wananchi wananufaika na rasilimali zao.



Kwa upande wake Sioi aliahidi kutekeleza ahadi zote zilizoachwa na mbunge aliyetangulia, ambaye ni baba yake mzazi, Marehemu Jeremiah Sumari.



Alisema atajikita kutatua tatizo la uhaba wa ajira kwa vijana ndani ya jimbo hilo kwa kushirikiana na Serikali bega kwa bega ikiwa ni pamoja na kuzindua vituo vya ujasiriamali kwa vijana ili waweze kujiajiri wenyewe badala ya kusubiri kuajiriwa serikalini.



“Nichagueni ili niweze kukamilisha ahadi zote zilizotolewa na mbunge aliyetangulia, nitajikita kutatua tatizo la ajira kwa vijana kwa kushirikiana na Serikali bega kwa bega,” alisema Sumari.



No comments:

LATEST NEWS

Share

Widgets

 

Total Pageviews