Social Icons

Sunday 18 March 2012

MWENYEKITI WA CCM KATA YA MBUGUNI AHAMIA CHADEMA

Katika hatua nyingine, Mwenyekiti wa CCM wa Serikali ya Kitongoji cha Madukani, eneo la Msitu wa Mbogo, Kata ya Mbuguni,Godzed Minja, juzi amerudisha kadi ya CCM na kujiunga na CHADEMA, wakati makada wa chama hicho wakimnadi Mgombea wao Nassari wilayani humo.


Akizungumza mara baada ya kujiunga na CHADEMA, Mwenyekiti huyo Minja, alisema kuwa amefanya uamuzi huo kutokana na kuona CCM haina sera zaidi ya kusambaza matusi na kashfa badala ya kujibu hoja za msingi.



“Mimi naahidi nitakuwa mwana Chadema safi na mwaminifu na sitarudi nyuma katika mapambano haya, CCM imepoteza mwelekeo,’’ alisema Minja.



Alisema kuwa atatumia muda wake mwingi kuhakikisha CCM katika Kata ya Mbuguni inapotea kabisa kwa sababu hawana sera za kuwaeleza wananchi juu ya ugumu wa maisha waliyosababisha na kuchangia viongozi wa chama hicho kupata wakati mgumu kwa Wananchi.



Naye Mchungaji Israel Natse, akizungumza wakati akimnadi Mgombea wao, Nassari alisema kuwa eneo la Msitu wa Mbogo, Kata ya Mbuguni CCM imekwisha kwa sababu wanachama wengi wamehama chama hicho na kujiungana Chadema, kutokana na sera zao za matusi mbele ya watoto wadogo.



Alisema kuwa wanachama zaidi ya 300 wanasubiri Katibu wa chama hicho Taifa Dk. Slaa na Mwenyekiti Freeman Mbowe, ili wakabidhi kadi hizo na kukabidhiwa kadi za Chadema mbele yao.



PIA Chadema yataka mdahalo huko Arumeru
Katika hatua nyingine Chadema, kimeomba kufanyika mdahalo wa wagombea wote wa ubunge wa jimbo la Arumeru Mashariki ili kutoa fursa kubwa kwa wapigakura wa jimbo hilo na Watanzania kwa ujumla, kuwafahamu.



Meneja Mwenza wa kampeni wa Chadema, Vincent Nyerere, alitoa ombi hilo jana katika mikutano ya kampeni ya chama hicho, katika Kijiji cha Kikatiti na Maleu, wakati mgombea ubunge wa chama hicho, Nassari akiomba kura.



Nyerere ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Musoma Mjini, alisema uchaguzi wa Jimbo la Arumeru Mashariki unasura ya kitaifa, hivyo ni busara kutoa fursa kwa Watanzania wengi kuwajua wagombea, sera zao na nini wamejipanga kuwafanyia wakazi wa jimbo hilo.



“Sisi Chadema tunataka wagombea wengine wakubali hasa CCM ambao wamekuwa wakikacha midahalo ili tutowe fursa kwa Watanzania kuwajua wagombea wao kwani kipindi cha kampeni ni kifupi sana, hivyo hakitowi nafasi wagombea kujulikana,”alisema Nyerere.



Awali Nassari aliwataka wakazi wa jimbo hilo kubadilisha siku ya kimataifa ya wajinga ambayo huadhimishwa Aprili mosi kila mwaka kuwa siku ya werevu kwa kuchagua kupinga maisha magumu, kupinga vitu kupanda bei na kupinga Meru kukosa ardhi na maji.



Nassari alisema, kumchagua yeye ni kuondoa shida na mateso yao yanayowakabili kutokana na serikali ya CCM kushindwa kutatua shida zao kwa miaka 50 sasa.



Mgombea huyo, aliendelea kusisitiza kuwa kati yawagombea wote, yeye ndiye anaishi Arumeru na ni mpiga kura wa jimbo hilo, hivyo anajua matatizo ya wakazi wa jimbo hilo.



“Mimi mimezaliwa Meru,nimesoma Meru,naishi Meru na ninafanya kazi Meru hivyo najua matatizo yenu na namna ya kuyatatua”alisema Nassari.




No comments:

LATEST NEWS

Share

Widgets

 

Total Pageviews