Social Icons

Sunday 18 March 2012

Lowassa,Mbowe vitani Arumeru

MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo, (Chadema), Freeman Mbowe amesema chama chake kinamgonja kwa hamu Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa katika kampeni za uchaguzi mdogo wa jimbo la Arumeru Mashariki mkoani Arusha.Kauli ya Mbowe inatokana na habari zilizoenea Arumeru ambazo pia zimethibitishwa na watu walio karibu na Lowassa, zikisema Mbunge huyo wa Monduli (CCM) wakati wowote atatua Arumeru Mashariki kumpigia kampeni mgombea wa chama chake, Sioi Sumari.

“Mzee (Lowassa) ni kweli kwamba ana mpango wa kuja hapa kumpigia kampeni mgombea wetu wa CCM, inaweza kuwa ni wiki ijayo au wiki ile nyingine, nadhani bado anajipanga. Ila taarifa za uhakika ni kwamba atakuja,”alisema mmoja wa makada wa CCM jana asubuhi.

Taarifa za kwamba Lowassa atashiriki kwenye kampeni hizo zilianza katikati ya wiki hii siku chache kabla ya kurejea kutoka Ujerumani.


Kwa upande wake, Lowassa akizungumza na Mwananchi kwa simu jana, hakuthibitisha wala kukanusha taarifa hizo, zaidi ya kusema kwamba hivi sasa anapumzika baada ya kurejea kutoka nchini Ujerumani alikokwenda kwa ajili ya matibabu ya macho.


“Kwani vipi……kwa kweli kwa sasa siwezi kusema lolote kuhusu hilo, ndiyo kwanza ninapumzika kama unavyojua nimetoka safari, katika hilo tusubiri kwanza,” alisema mbunge huyo ambaye anatajwa kwamba alikuwa akimuuga mkono Sioi kuanzia kwenye mchakato wa kura za maoni ndani ya CCM.

Kwa upande wake Mbowe akizungumzia taarifa za ujio wa Lowassa alisema: “Tunamsubiri sana kwa hamu, kwani yeye ni nani? Lowassa ni kama mtu mwingine yoyote ndani ya CCM, hivyo yoyote atakayeletwa na CCM wala hatumwogopi, tuko tayari kukabiliana naye.”

Aliongeza: “Kwani Mkapa (Benjamin) si alikuja hapa….akamuulize baada ya kuzindua kampeni za chama chake na kusema maneno yake kilichomtokea ni nini? Kwa hiyo bwana na yeye (Lowassa) ni walewale maana hana tofauti na Mkapa maana wote wanatoka CCM, sisi Chadema hatutishiki hata kidogo.”

Lowassa ni miongoni mwa wazaliwa wa mkoani Arusha wanaotajwa kwamba wanakubalika katika siasa za Arumeru, hivyo ujio wake unaweza kuwa chachu kubwa katika kampeni za CCM kinachopigania kuendelea kushika nafasi ya uwakilishi wa jimbo hilo.

Wakati hayo yakiendelea, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa anatarajiwa kutua Arumeru leo kuongeza nguvu katika kampeni za Chadema ambacho kinawania kujenga heshima kwa mgombea wake, Joshua Nassari kutwaa jimbo hilo.

Tayari CCM wameongeza nguvu za kampeni zake kwa kuwaogeza makada kadhaa, wengi wakiwa ni wabunge wa majimbo mbalimbali wanaoongozwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Stephen Wasira, hivyo kuongeza chachu ya kampeni hizo.

No comments:

LATEST NEWS

Share

Widgets

 

Total Pageviews