Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amerejea Dar es Salaam mchana wa jana, Jumanne,
baada ya kumaliza ziara ya siku tisa katika mikoa minne ambako amekagua,
kuanzisha ama kuzindua miradi 19 ya maendeleo na kutembea kiasi cha kilomita
2,770.
Rais Kikwete amewasili Dar es
Salaam akitokea Dodoma ambako amefanya ziara ya kikazi ya siku mbili baada ya
kumaliza ziara katika mikoa ya Kilimanjaro, Arusha, Manyara na
Singida.
Katika Mkoa wa Kilimanjaro ambako
Rais Kikwete alianzia ziara yake Oktoba 28, mwaka huu, miongoni mwa mambo
mengine alikagua nyumba za wahanga wa maporomoko ya mwaka 2006 kwenye kijiji cha
Goha na akafungua Kiwanda cha Kusindika Tangawizi kilichoko Mamba Miamba, Wilaya
ya Same, na akafungua Shule ya Sekondari ya Kata ya Asha Rose Mingiro iliyoko
mjini Mwanga.
Miradi mingine aliyoifungua Rais Kikwete katika
Mkoa wa Kilimanjaro ni uzinduzi wa barabara za Rombo Mkuu-Tarakea na
Kwasadallah-Masama na akafungua Ofisi ya Mkaguzi Mkuu na Mdhibiti wa Hesabu za
Serikali (NAO) mjini Moshi.
Katika Mkoa wa Arusha, Rais Kikwete alizindua
Hospitali ya Wilaya ya Arusha ya Olturumet, akazindua Mradi Mkubwa wa Uboreshaji
wa Miji kwa kufungua barabara za Jiji la Arusha, akazindua Jiji la Arusha,
akafungua rasmi Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Nelson Mandela na
akatembelea Kiwanda cha Nguo cha A-Z.
Kabla ya kuondoka Mkoani Arusha, Rais Kikwete
alifungua Shule ya Msingi ya Sokoine na kuzindua ukarabati mkubwa wa Barabara ya
Minjingu-Arusha.
Mkoani Manyara, Rais Kikwete alifungua rasmi
Barabara ya Singida-Minjingu-Arusha, akazindua mradi mkubwa wa maji wa Mji wa
Babati na akaweka jiwe la msingi kwenye ujenzi wa Barabara ya
Babati-Bonga.
Mkoani Singida, Rais Kikwete alizindua mradi
mkubwa wa maji wa Mwankoko kwa ajili ya Mji wa Singida, akaweka jiwe la msingi
kwenye ujenzi wa Barabara ya Manyoni-itigi-Chaya na akafungua Barabara ya
Issuna-Manyoni.
Imetolewa
na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya
Rais,
Ikulu.
Dar es
Salaam.
6 Novemba, 2012
No comments:
Post a Comment