Social Icons

Thursday 9 February 2012

Mgomo wa madaktari, Suluhu yapatikana baada ya mazungumzo.


Waziri Mkuu Mizengo Pinda amewasimamisha kazi Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii Blandina Nyoni na Mganga Mkuu wa Serikali Dokta Deo Mtasiwa ili kupisha uchunguzi kuhusu chanzo cha mgomo wa Madaktari unaoendelea.
Hata hivyo Waziri Mkuu Pinda amemwachia Rais Jakaya Kikwete uamuzi wa mwisho kuhusu hatma ya Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Dokta Haji Mponda na Naibu wake Dokta Lucy Nkya ambao pia wanalalamikiwa na Madaktari kwa madai ya kupuuza malalamikoyao.
Mapambazuko ya asubuhi ya Alhamisi yanamkuta Waziri Mkuu Mheshimiwa Mizengo Pinda kwenye Hospitali ya Taifa ya Muhimbili lengo kuu likiwa ni kutatua mgogoro baina ya serikali na madaktari.
Ni siku ya 17 tangu mgogoro huo uanze na mashinikizo yamekuwa yakiongezeka kila kona huku kukiwa na tetesi kuwa baadhi ya Mawaziri walimtaka mwenzao Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Dokta Haji Mponda kujiuzulu kutokana na sakatahilo.
Waziri Mkuu amefika katika hospitali hiyo majira ya saa 3 asubuhi huku mamia ya madaktari wakimsubiri kwa hamu kujibu madai waliyomuwasilishia mezani likiwemo lile la kuwawajibisha viongozi wakuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kwa madai ya kutowasikiliza na kuwapuuza pindi wanapowasilisha madaiyao.
Miongoni mwa madai ya madaktari hao ni kupewa kipaumbele kwa madaktari walio kwenye mafunzo kwa vitendo, kuongezewa posho za muito wa ziada yaani (on call allowance), Posho za nyumba au kupewa nyumba, posho za mazingira hatarishi, usafiri na kuongezewa mshahara.
Pamoja na yote aliyowaahidi Waziri Mkuu ametoa mwito kwa madaktari hao kurejea kazini ili kuwasaidia wagonjwa wanaoteseka kwa kukosa hudumayao.
Mbali na masuala ya mishahara Waziri Mkuu pia ameahidi kuboresha mazingira ya kazi, mazingira ya afya mahospitalini, kuongeza vitendea kazi na kuwaongezea posho za mwito wa dharura yaani (on call allowance) kutoka shilingi 10,000/- mpaka shilingi 25,000/-.
Masuala mengine yasiyotatulika kwa haraka, Waziri Mkuu ameyaundia tume ya watu 9 itakayofuatilia na kumpelekea ripoti, tume hiyo imeshirikisha wawakilishi kutoka Chama cha Madaktari MAT, Chama cha wafanyakazi wa serikali kuu na afya TUGHE, mwakilishi kutoka Hazina, Wizara ya Afya na idara zingine kutoka serikalini na vyama vya wafanyakazi.
Kwa upande wao madaktari wameomba wapewe muda mzuri zaidi kwa ajili ya kuendelea kujadili masuala mbalimbali yanayowakabili.
Hata hivyo mpaka kikao kinamalizika madaktari hao wamekubaliana kusitisha mgomo na kurejea kazini kwa ajili ya kuendelea na kazi huku wakitarajia kukutana tena Mwezi ujao tarehe 3 mwaka huu kuangalia masualayaoya kikazi.
Mgogoro huo uliochukua takriban wiki tatu mfululizo umeanza baada ya Wizara ya afya kuchelewesha posho za Madaktari Wanafunzi hatua iliyowafanya wasitishe huduma katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili na kuanza kuitisha vikao kupitia kwa Chama cha Madaktari Tanzania MAT ambavyo viliibua madai mengine ya nyuma.

No comments:

LATEST NEWS

Share

Widgets

 

Total Pageviews