Social Icons

Friday 24 February 2012

Haji Salum ‘Mboto’: Mr Bean wa Bongo mwenye ndoto ya kung’aa kimataifa


 KATIKA fani ya uigizaji, mbali na kipaji lakini pia namna msanii anavyobeba uhusika wa nafasi anayoigiza huwa ni mambo yanayomvutia mtazamaji.

Uwezo wa msanii utapimwa kutokana namna alivyoweza kuuvaa uhusika mfano anapotakiwa kuigiza kama ana huzuni lazima aoneshe hali ya huzuni, kama anaigiza tajiri aonekane kweli tajiri, kichaa kweli aonekane mgonjwa wa akili na kama anapaswa kuwa mchekeshaji basi awe mchekeshaji kweli. 
Uwezo wa kubeba uhusika vizuri ndio huko kunakomfanya msanii wa vichekesho Haji Salum maarufu kwa jina la Mboto kuweza kung’ara katika fani ya filamu za vichekesho. Anasema, “Ninakuwa na wakati mgumu sana wakati wa kuandaa kazi, tunalazimika kurudia mara kwa mara.


Si kwa sababu hatuwezi kuigiza, ni kutokana na wasanii wenzangu kushindwa kuvumilia vichekesho vyangu.” Safari ya Mboto haikuwa rahisi, anasema amefika hapo kutokana na uwezo wake wa kujiamini na kupenda kujifunza kutoka kwa watu wengine.

Uwezo wa Mboto ndio unaomfanya kupewa nafasi kushiriki kwenye nyimbo za wasanii wa kizazi kipya akiwakilisha maudhui ya wimbo huo kwa njia ya vitendo na wakati mwingine vichekesho.

Baadhi ya nyimbo ambazo ameshiriki vilivyo ni pamoja na ‘Utaipenda” wa Hussein Machozi ambao waliweza kufanya vizuri, ‘Iveta’ wa Sajna ambapo amefanikiwa kuipendezesha video hiyo kutokana na uwepo wake na ‘Starehe Gharama’ wa Tunda Man ambapo Mboto ameifanya video hiyo ionekane imekaa vyema.

“ Sanaa yangu ni ya kujifunza kutoka kwa watu wengine, pamoja na kuijua sanaa lakini sijui kuimba na sina hata sauti ya kuimba ingawa mama yangu alikuwa mpenzi sana wa kuimba na alikuwa na sauti nzuri, “ anasema.

Tofauti na wasanii wengine, Mboto anaonesha uwezo mkubwa na kuuvaa uhalisia vizuri pindi anapofanyakazi ya uchekeshaji na hata filamu za kawaida jambo ambalo limefanya baadhi ya mashabiki wake kumuita Mr. Bean wa Bongo huku wengine wakimuita muuza sura. Ikiwa ni tofauti na mtazamo wa baadhi ya mashabiki wake kumuita Mr. Bean wa Bongo, Mboto anavutiwa na kutamani kufuata nyanyo za msanii wa Marekani, muigizaji Will Smith ambaye ana uwezo wa kuigiza vizuri filamu za kawaida na vichekesho.

“Unajua Smith ni msanii anayeweza kuigiza filamu ‘serious’ na zile za komedi, kutokana na uwezo nilionao naweza kujifananisha naye na napenda kufikia kiwango chake kwa kuwa matarajio yangu ni kuwa msanii wa kimataifa,” anasema Mboto. Akizungumzia sanaa ya uchekeshaji hapa nchini, Mboto anasema tofauti na miaka ya nyuma ambapo wasanii wa uchekeshaji walikuwa wanadharauliwa, sasa wameboreshewa malipo ambapo wanalipwa sawa sawa na waigizaji wengine kwa kuweka makubaliano na mwenye filamu.

“Zamani mtu wa uchekeshaji alikuwa anashirikishwa kwa malipo ya Sh 3000 au hata 5000 na kutakiwa kucheza kipande kifupi na hapo uhusika wako unaisha. Ilikuwa njaa tupu lakini kwa sasa kazi na mchango wetu unatambulika katika jamii na tunapewa haki sawa kama wengine,”anasema.

Mboto alianza sanaa ya uigizaji akiwa shule ya msingi ambapo alikuwa akishiriki katika michezo ya aina mbalimbali na baadaye kufanya kazi ya uigizaji kwa muda kipindi cha vichekesho cha Mizengwe kinachorushwa na Kituo cha Televisheni cha ITV. “ Nikiwa Mizengwe ndipo Max (marehemu) na Zembwela waliponitungia jina la Mboto na halikuwa na maana yoyote ile.

Lakini katika kujitafutia maisha niliamua kujiunga na kundi la sanaa la Kaole,” anasema msanii huyo. Alipojiunga na Kaole mwaka 1999 ndipo hasa kipaji chake cha uchekeshaji kilipozidi kukua na kuonekana na baadaye kuongoza jopo la wale wanaosaili wachekeshaji waliokuwa wakitaka kujiunga katika kundi hilo.

Anapozungumzia vikwazo anavyokutana navyo katika sanaa, Mboto anasema kuwa tatizo ni mauzo, wasanii kutopendana, hawataki kuoneshana njia na hawataki kuoneshana masoko. “ Yani unaweza kukuta mtu amefanikiwa lakini ukimuuliza hataki kukuelekeza ufanye nini ili ufanikiwe hasa watu wa komedi,” anasema kwa masikitiko.

Mboto anasema lengo lake ni kuwa msanii wa kimataifa na kwamba anataka kazi zake zitambulike na anaongeza kuwa atalifanikisha hilo kwa kufanya kazi bora kwa kushirikiana na wasanii wenye uwezo (sio kutokana na majina). (nataka wasiseme nimebahatisha bali nitoke kutokana na uwezo wangu,” anasema.

Aidha, anasema wasanii wenye tabia ya kuiga maudhui na uigizaji kutoka kwenye filamu za nje siyo wabunifu na hawaamini uwezo wao na hakika kazi zao zitaishia hapa hapa. “ Hebu angalia filamu ya Terminator ambayo mpaka leo bado inapendwa kwa kuwa aliyeitengeneza alikuwa na malengo na ajenda isiyoisha leo, “ anasema Mr Bean wa Bongo.

Mboto anasisitiza zaidi, “Nikifanya kazi na msanii JB kwa upande wa filamu za umakini na Kingwendu kwa filamu za komedi huwa najisikia vizuri sana na ndio wasanii ninaowakubali.” Anapozungumzia tatizo la wizi wa kazi za wasanii, Mboto anaitaka Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) kuingilia kati katika kusimamia uuzwaji wa kazi zao kwa kuweka nembo maalumu.

“TRA watusaidie kwa hili, waweke nembo ambazo wao watadhibiti na hata kama kukatwa Sh 300 kwa kila kanda moja, mchango huu wa wasanii uweze kuongeza pato la Taifa,” anasema. Mboto ambaye ni muigizaji na mtunzi wa filamu nyingi ikiwa ni pamoja na Mtoto wa Nyoka, Maamuzi, King Mwalubadu na nyingine nyingi amewataka wasanii wanaochipukia wasitafute umarufu bali watambue sanaa ni kazi kwa kutengeza filamu zenye maudhui ya kuchekesha na sio za kuanza na kuisha.

“Nimefanya kazi nyingi za filamu ambazo si za vichekesho, lakini filamu ya ‘Nampenda Mke Wangu’ ndiyo filamu ambayo ninaona kazi niliyoifanya ilikuwa kubwa na iliweza kunionesha kuwa si vichekesho pekee ninavyoweza kuigiza,” anasema. Akizungumzia jambo lililomhuzunisha, Mboto anasema,” siku mama yangu alipofariki dunia. Yaani tukio hili siku zote linanikumbusha usemi wake wa usiwe na nyota ya paka kupendwa na wachawi.”

Anafafanua usemi huo kuwa ni “nisiwe na nyota ya kupendwa na watu wasiopenda maendeleo”. Akizungumza na Bongo5 hivi karibuni Mboto alisema lengo lake ni kushawishi wasanii wanaofanya vichekesho vya kujidhalilisha kwa kuvaa matambara waache na wairudie sanaa kwa usafi na ustaarabu.

Anasema watazamaji wa sasa sio wale wa mwaka 47, wa sasa wapo kisasa zaidi na kwamba wanataka pia kuona mtiririko mzima wa matokeo na sio vipande vya maongezi ya kuchekesha. "Nataka kufanya mabadiliko kwenye tasnia ya vichekesho, kwa kufanya mfululizo (series) wa matukio na sio vipande vya maongezi kama ilivyokuwa zamani,” anasema.

Mboto anasema changamoto inayowakabili wasanii wa komedi nchini ni ukosefu wa elimu ya darasani na mtaani pia na ndio maana wanaonekana kama vile ni watu wasio na umuhimu katika tasnia hii.

No comments:

LATEST NEWS

Share

Widgets

 

Total Pageviews