Social Icons

Saturday 4 February 2012

Wabunge wazuiwa kujadili mgomo wa madaktari

WABUNGE leo wamezuiwa kujadili kauli ya Serikali kuhusu namna ilivyoshughulikia mgomo wa madaktari.

Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai, amewaeleza wabunge kuwa, si busara kuijadili kauli hiyo kwa kuwa wamesikia upande mmoja tu wa Serikali, hawajasikia upande wa madaktari wanasema nini.

Ndugia amekiri kwamba suala ni nyeti kwa kuwa linahusu maisha na uhai wa wananchi wanaohitaji tiba lakini taratibu za uendeshaji wa mabunge ya Jumuiya ya Madola haziruhusu kujadili kauli za mawaziri mara tu baada ya kuwasilishwa.

Amesema kutojadili kauli hizo moja kwa moja kunaepusha kauli tofauti tofauti.

Kwa mujibu wa Ndugai, si busara kwa wabunge kuijadili kauli ya Serikali iliyowasilishwa leo bungeni na Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Haji Mponda.

Ndugai amesema , madaktari hawajasikilizwa na hawawezi kwenda bungeni kutoa kauli yao lakini licha ya madai mengine, wanawatuhumu watendaji wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii hawawajibiki na wanatoa kauli za kashfa hivyo si busara kwa wabunge kulijadili suala hilo.

“Sijui kama tutakuwa tunajitendea haki hata sisi wenyewe unless ( isipokuwa) kama tupo informed (kuwa na uelewa wa kutosha kuhusu jambo fulani” amesema Ndugai.

Ametoa msimamo huo wakati anatoa mwongozo wake kuhusu hoja ya Mbunge wa Ubungo, John Mnyika (Chadema) ya kuomba Bunge lijadili kauli ya Serikali kuhusu namna ilivyoshughulikia mgomo wa madaktari.
Mnyika amesema, ni busara kwa wabunge kuijadili kauli hiyo kwa kuwa, Serikali ni moja ya pande zinazohusika kwenye mgororo huo,hivyo ni busara kauli iliyotoa ijadiliwe na wahusika wawajibishwe.
Mbunge huyo aliomba mwongozo huo kabla Waziri Mponda hajawasilisha kauli hiyo, na baada ya kuwasilishwa, Mbunge wa Kasulu Mjini, Moses Machali (NCCR- Mageuzi), na Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto (Chadema) nao waliomba kauli ya Serikali ijadiliwe. Baada ya Ndugai kutoa mwongozo huo aliiagiza Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma za Jamii izungumze na Serikali na madaktari ili kumaliza mgogoro huo.

Ameitaka kamati hiyo hiyo ifanye kazi hiyo haraka na itoe taarifa kuhusu yaliyojiri kwenye mazungumzo hayo na ushauri wa Bunge kwa pande husika.
Amesema, ushauri wa Bunge kwa pande hizo si lazima yawe maagizo, na kwamba, wabunge wanaruhusiwa kuhudhuria vikao vya kamati na pande husika, na kuchangia.

No comments:

LATEST NEWS

Share

Widgets

 

Total Pageviews