Social Icons

Friday 24 February 2012

Precision Air yabadili ratiba ya Afrika Kusini



SHIRIKA la Ndege la Precision Air, limetangaza kufanya  mabadiliko katika ratiba yake ya safari kwenda Johannesburg nchini Afrika Kusini, ambapo itaanza kuondoka saa 11 jioni badala ya saa mbili usiku ili kuwawezesha wasafiri wake kuwahi na kuwapatia urahisi wa kuunganisha safari kwenda kwingine.

Akizungumza katika makao makuu ya Precision Air, Dar es Salaam jana, Kaimu Mkurugenzi wa Biashara, Patrick Ndekana alisema uamuzi huo umekuja baada ya utafiti uliofanywa na shirika hilo, uliopendekeza watumiaji wa huduma hiyo wanapendelea kusafiri mapema ili kupata urahisi wa kuunganisha safari kwenda kwingine pamoja na kujihakikishia usalama kwa wanaoishia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Oliver Tambo.



“Kuanzia Februari 29 mwaka huu, tutaanza kuondoka Dar es Salaam saa 11 jioni na kufika jijini Johannesburg saa 1:45 usiku,” alisema Ndekana.

Alisema pamoja na kufanyika kwa mabadiliko hayo, muda wa kurejea kutoka Johannesburg kwenda Dar es Salaam hautabadilishwa.

“Muda wa kutokea Johannesburg utabakia pale pale saa 5:50 usiku na kufika Dar es Salaam saa 10:20 alfajiri,” alisema Ndekana.

Kwa mujibu wa Ndekana, mabadiliko hayo yanaashiria pia kwamba Precision Air wana umakini wa kusikiliza na kuchukulia maanani mawazo mbalimbali kutoka kwa wateja wake.

“Kama shirika la umma iliyoorodheshwa katika Soko la Hisa la Dar es Salaam kupokea maoni mbalimbali kutoka kwa wanahisa na wadau wetu ni jambo jema, ambayo tunaamini kwamba inatuongezea thamani kubwa kama shirika la ndege,” alisema Kaimu Mkurugenzi wa Biashara.

Katika hatua nyingine, Precision Air ikishirikiana na Shirika la Ndege la Kenya (Kenya Airways), imeongeza idadi ya safari za moja kwa moja baina ya Dar es Salaam na Nairobi kutokea nne hadi tano kwa siku.

Akizungumzia nyongeza hiyo, Kaimu Mkurugenzi wa Biashara wa Precision Air, alisema safari hizo zitafanyika kwa kushirikiana na Kenya Airways, ambao wataratibu safari mbili wakitumia ndege aina ya Embraer 190 (E190) wakati Precision Air wataratibu safari tatu kutumia ndege yao ya B733.

Alisema safari ya nyongeza ya Nairobi kutokea Dar es Salaam inatarajiwa kuanza sawia na mabadiliko ya safari ya Johannesburg, Februari 29, mwaka huu.

Precision Air ina mtandao mkubwa nchini kuliko mashirika yote Tanzania ikiwa inafanya safari kwenda Dar es Salaam, Arusha, Kilimanjaro, Zanzibar, Mwanza, Bukoba, Kigoma, Tabora, Musoma, Shinyanga na Mtwara. Kikanda Precision Air inasafiri kwenda Nairobi, Mombasa, Entebbe, Hahaya na Johannesburg.

No comments:

LATEST NEWS

Share

Widgets

 

Total Pageviews